Sunday, July 5, 2015

FIJI YASHINDA MABAO 38-0 KATIKA MCHEZO WA SOKA.

KISIWA cha Fiji kimefanikiwa kuvunja rekodi kubwa katika historia ya michuano ya bara la Pacific kwa ushindi wa mabao 38-0 dhidi ya Micronesia leo. Katika mchezo huo Fiji ilifunga mabao 21 katika kipindi cha kwanza huku mengine 17 wakimalizia katika kipindi cha pili na Atonio Tuivuna akiibuka shujaa wa mchezo kwa kufunga mabao 10 peke yake. Ushindi huo umeifanya Fiji kupata matumaini ya kufuzu michuano ya Olimpiki itakayofanyika jijini Rio de Janeiro mwakani pamoja na kwamba Micronesia sio mwanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki-IOC. Hiyo ni mara ya pili kwa Micronesia kupokea kipigo kizito katika michuano hiyo ya ukanda wa Oceania baada ya siku mbili zilizopita kutwishwa mabao 30-0 na Tahiti hivyo kuzima ndoto zao za kusonga mbele katika kundi A. Hata hivyo kutokana na Micronesia kutokuwepo katika orodha za viwango vya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Australia ndio itabakia nchi pekee katika historia kupata matokeo makubwa katika mchezo wa kimataifa waliopoitandika Samoa kwa mabao 31-0 katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2002.

No comments:

Post a Comment