Tuesday, April 29, 2014

BAYERN WATAIFUNGA MADRID - NEUER.

GOLIKIPA wa Bayern Munich, Manuel Neuer ana uhakika timu yake inaweza kutinga hatua ya fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuing’oa Real Madrid. Madrid waliibuka kidedea kwa kushinda bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Santiago Bernabeu wiki iliyopita na timu hizo zinatarajia kurudiana tena leo. Hata hivyo, Neuer anaamini kuwa uzoefu wa Bayern kutinga hatua hiyo utawasaidia kuifunga Madrid ambao wameshindwa kupenya kutoka katika hatua hiyo kwa misimu mitatu iliyopita. Neuer alitamba kuwa wana silaha zilizo katika hali nzuri na ana uhakika wataifunga Madrid.

TERRY, CECH FITI KUIVAA ATLETICO.

GOLIKIPA Petr Cech na beki John Terry wameanza mazoezi na timu yao leo kuelekea mchezo wa marudiano wa nusu fainali dhidi ya Atletico Madrid kesho. Ilisemekana Cech asingeweza kucheza tena msimu huu baada ya kuteua bega lake katika mchezo wa kwanza wakati Terry alitolewa nje kutokana na kuumia kifundo cha mguu katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 0-0. Eden Hazard na Samuel Eto’o ambao walikuwa majeruhi wao pia walionekana kuwa fiti kwa kufanya mazoeziya leo. Viungo John Mikel Obi na Frank Lampard wote hawatakuwepo katika mchezo huo wa marudiano utakaofanyika katika Uwanja wa Stamford Bridge kutokana na kutumikia adhabu ya mechi moja.

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa ya Mikoa-RCL msimu wa 2013-2014 inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 10 mwaka huu katika vituo vitatu vitakavyokuwa na timu tisa kila kimoja. Katika taarifa taarifa ya TFF iliyotumwa kwa vyombo vya habari, imedai kuwa mechi za michuano hiyo zitachezwa kwa mkondo mmoja katika vituo ambavyo ni Mbeya, Morogoro na Shinyanga. Mshindi katika kila kituo cha ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Juni 2 mwaka huu atakuwa amekata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi Daraja la Kwanza-FDL kwa msimu wa 2014-2015. Wakati huohuo timu ya taifa ya Malawi inatarajiwa kuwasili nchini Mei mosi kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Taifa Stars utakaochezwa Mei 4 mwaka huu katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Mchezo huo utakuwa mahsusi kwa ajili ya Stars inayonolewa na kocha mpya Mart Nooij kujiandaa na mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Zimbabwe utakaochezwa kati ya Mei 16 na 18 mwaka huu.


REUS ACHOSHWA NA MASWALI YA MKATABA MPYA.

MSHAMBULIAJI wa Borussia Dortmund, Marco Reus amedai kuchoshwa na maswali kuhusu mustakabali wake na kukataa kuthibitisha kama amepewa ofa ya mkataba mpya. Kuna tetesi kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 amepewa ofa ya mkataba mpya ambao utaifanya thamani yake kupaa mpaka euro milioni 35 kwa timu nyingine itakayimhitaji. Hata hivyo, wakati akihojiwa kuhusiana na makubaliano hayo, Reus alikataa kusema chochote kuhusiana na suala hilo. Reus amesema hatasema chochote kuhusiana na mkataba wake lakini ana muda wa kuzungumzia kuhusu anavyojisikia vyema akiwa klabuni hapo.

KIPIGO CHAWAVURUGA MASHABIKI WA NEWCASTLE.

MENEJA wa klabu ya Newcastle United, Alan Pardew bado anaamini anaweza kubakia kwa muda mrefu kuifundisha timu hiyo pamoja na kupoteza mechi sita mfululizo na kusababisha mashabiki kuchukizwa. Mashabiki hao wa Newcastle wameonyesha hasira zao kufuatia kipigo cha mabao 3-0 walichopata kutoka kwa Arsenal jana usiku. Akihojiwa Pardew amesema anajua mashabiki hao wamehuzunishwa na kukasirishwa hivi sasa kwasababu hawajapa matokeo mazuri lakini ameomba uvumilivu kwani ana mipango ya muda mrefu na timu hiyo. Newcastle walianza vyema msimu mpaka kumalizika kwa mzunguko wa kwanza lakini walionekana kuporomoka toka kuanza kwa mwaka huu mpaka kufikia nafasi ya nane waliyopo hivi sasa.

WADHAMINI WA LA CLIPPERS WAJITOA KUTOKANA NA KAULI YA YA KIBAGUZI YA MMILIKI WAKE.

BAADHI ya wadhamini wa timu ya mpira wa kikapu ya Marekani, Los Angeles Clippers wamejitoa baada ya mmiliki wa timu hiyo kutuhumiwa kutoa kauli za kibaguzi. Chama cha Soka nchini humo-NBA inachunguza kauli hiyo ambayo inadaiwa kutolewa na Donald Sterling mwenye umri wa miaka 80. Wadhamini wanne ikiwemo kampuni ya Marcedes Benz ya Marekani wamesitisha udhamini wao wakati kampuni ya vinywaji ya Red Bull wakiwa mojawapo ya makampuni yaliyosimamisha matangazo yao. Wachezaji wa Clippers walifanya maandamano ya kimya kimya Jumapili kwa kuvaa fulana zao wakiwa wamezigeuza ndani-nje wakati wakipasha misuli yao moto kabla ya mechi dhidi ya Golden State Warriors.

UEFA YAWATIA KITANZI MAN CITY NA PSG KWA KUKIUKA SHERIA ZA MATUMIZI YA FEDHA.

KLABU za Manchester City ya Uingereza na Paris Saint-Germain ya Ufaransa watakabiliwa na adhabu baada ya kukiuka maadili ya sheria ya matumizi ya fedha ya Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA. Mbali na hao vilabu vingine vipatavyo 20 vinaaminika kukutwa na hatia ya kuvunja sheria hiyo. UEFA itatoa ofa maalumu kwa vilabu hivyo vilivyokiuka sheria hiyo kuelekea katika mkutano wao utakaofanyika Alhamisi. Adhabu kubwa ambayo ni timu husika kuenguliwa katika michuano ya Ulaya haitarajiwi kuwepo ingawa pia hawakuweka wazi ni adhabu zipi zitaazotolewa kwa timu hizo.

VILANOVA AAGWA KWA MISA MAALUMU BARCELONA.

WACHEZAJI wa klabu ya Barcelona jana walionekana katika majonzi makubwa wakati wa misa ya kumuaga kocha wao wa zamani Tito Vilanova aliyefariki akiwa na umri wa miaka 45. Kikosi chote cha wachezaji wa timu hiyo, familia ya wafiwa na baadhi watu mashuhuri katika soka walihudhuria misa hiyo iliyofanyika katika kanisa la Cathedral jijini Barcelona. Vilanova ambaye aliiongoza Barcelona kushinda taji la La Liga msimu uliopita alifariki dunia Ijumaa wiki iliyopita baada ya kuugua saratani ya koo. Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu aliongoza ujumbe wa viongozi wa zamani wa timu hiyo wakiwemo Joan Laporta na Sandro Rosell huku vilabu vingine vya La Liga vikituma uwakilishi katika misa hiyo. Zaidi ya watu 50,000 walitembelea eneo maalumu lililotengwa katika Uwanja wa Camp Nou kwa ajili ya kutoa heshima zao kwa kocha huyo.

WENGER AKIRI MAJERUHI NDIO CHANZO CHA TIMU YAKE KUPOROMOKA.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amekiri kuwa majeruhi ya mara kwa mara kwa nyota wake ndio yaliyochangia kwa kiasi kikubwa kushindwa mbio za kugombea taji la Ligi Kuu. Arsenal ambao jana wameinua matumaini yao ya kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi baada ya kuichabanga mabao 3-0 Newcastle United wamekuwa wakisumbuliwa na majeruhi kwa nyota wake akiwemo Aaron Ramsey ambaye alikuwa nje kwa kipindi kirefu. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Wenger amesema suala la majeruhi limekuwa tatizo kubwa kwake kwani aliwapoteza wachezaji wake nyota katika kipindi muhimu cha msimu. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa ushindi dhidi yaNewcastle ulikuwa ni muhimu sana kutokana na malengo yao waliyojiwekea. Arsenal sasa wametofautiana na Everton waliopo nafasi ya tano kwa alama nne na wakipata ushindi wa mechi moja watakuwa wamejihakikishia nafasi hiyo.

SIMEONE AIGWAYA CHELSEA.

MENEJA wa klabu ya Atletico Madrid, Diego Simeone anaamini ushindi wa Chelsea dhidi ya Liverpool bila kuwa na baadhi ya nyota wake unaonyesha jinsi gani wanaweza kuwadhuru wakati watakapokutana katika mchezo wao wa marudiano kesho. Timu hizo mbili zinaingia katika mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kutoka sare ya bila ya kufungana Jumanne iliyopita. Simeone amesema ni wazi Chelsea wana timu kubwa kwasababu wameshinda pamoja na kufanya mabadiliko mengi, hiyo inamaanisha watakwenda kucheza na timu yenye nguvu. Atletico wataingia kutafuta nafasi ya kucheza fainali ya kwanza ya michuano hiyo toka mwaka 1974 wakati walifungwa na Bayern mabao 4-0 huko Heysel.

Monday, April 28, 2014

KLOPP AWAPA NAFASI MAHASIMU WAO BAYERN KUTINGA FAINALI LIGI YA MABINGWA ULAYA.

MENEJA wa klabu ya Borussia Dortmund, Jurgen Klopp ameipa nafasi Bayern Munich kugeuza matokeo ya kufungwa bao 1-0 na Real Madrid katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bao la Karim Benzema lilitenganisha timu hizo mbili katika mchezo huo uliofanyika wiki iliyopita katika Uwanja wa Santiago Bernabeu baada ya Madrid kucheza mchezo wa tahadhari kubwa. Hata hivyo, Klopp ambaye timu yake ilienguliwa na Madrid katika mzunguko wa mwisho anaamini mahasimu wao Bayern watashinda mchezo huo. Klopp amesema bado anashawishika kuamini kuwa Bayern wanaweza kushinda hususani kwa mchezo maridadi waliouonyesha mara ya kwanza pamoja na kufungwa. Bayern na Madrid zinatarajiwa kukwaana kesho katika mchezo wa marudiano kutafuta nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo itakayofanyika jijini Lisbon, Ureno.

WACHEZAJI WA LOS ANGELES CLIPPERS WAFANYA MAANDAMANO YA KIMYA KIMYA KUFUATIA KAULI YA KIBAGUZI YA BOSI WAO.

WACHEZAJI wa mpira wa kikapu nchini Marekani wamefanya maandamano ya kimya kimya kufuatia ripoti kuwa mmiliki wa timu yao amerekodiwa kisiri akitoa kauli za kibaguzi. Los Angeles Clippers waliingia kupasha misuli moto jana huku fulana zao wakiwa wamezigeuza ndani-nje ili kuficha nembo ya timu hiyo. Chama cha Mpira wa Kikapu nchini Marekani-NBA kinachunguza taarifa hiyo iliyotolewa na mtandao wa habari za mastaa wa TMZ kuwa mmiliki wa Clippers Donald Sterling ndio aliyetoa kauli hiyo. 
Wachezaji wa timu hiyo walivaa vita vyeusi mikononi huku wote wakivaa soksi nyeusi katika jezi zao za kawaida. Sterling aliinua Clippers mwaka 1981 na hakuwepo katika mchezo huo dhidi ya Golden State Warriors uliofanyika jijini Oakland ambao wachezaji wake walifanya mgomo huo wa kimya kimya.

DEL PIERO AAMUA KUTUNDIKA DARUGA.

MCHEZAJI mkongwe Alessandro Del Piero ameamua kutundika daruga kuitumikia klabu ya Sydney FC lakini anaweza kurejea kwa shughuli nyingine. Nguli huyo wa zamani wa Juventus amekuwa akihusishwa na tetesi za kuwa kocha katika klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchiniAustralia maarufu kama A-League baada ya Frank Farina kutimuliwa. Del Piero mwenye umri wa miaka 39 na klabu hiyo wanataka kuendelea na mahusiano lakini haijabainika wazi ni uhusiano wa namna gani. Baada ya kufunga mabao 24 ambayo yamemfanya kumaliza kama mfungaji bora wa klabu katika misimu yote miwili aliyoitumikia, Del Pierro ametoa ujumbe wa kushukuru na kuaga katikamtandao wake. Del Piero amesema katika ujumbe huo ule wakati umewadia safari yake akiwa na Sydney FC inakaribia ukingoni ingawa inasikitisha lakini amekuwa na muda mzuri katika kipindi chote alichoitumikia.

NEYMAR AAPA KUPAMBANA NA UBAGUZI WA RANGI.

MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Neymar ameapa kupambana na unyanyasaji wa kibaguzi baada ya mchezaji mwenzake Dani Alves kutupiwa ndizi wakati wa mchezo wa La Liga dhidi ya Villarreal ambao walishinda maba 3-2 Jana. Beki huyo wa kimataifa wa Brazil alichukulia tukio hilo kwa utulivu kwa kuchukua ndizi hiyo aliyorushiwa na kuila lakini Neymar alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kukemea tukio hilo. Neymar aliandika katika katika mtadao wake huo kuwa watu wote ni sawa, wote ni nyani kemea ubaguzi wa rangi. Nyota huyo aliendelea kudai kuwa ni aibu kwa karne hii watu kuendelea na vitendo hivyo, ni wakati wa watu kupaza sauti na kukemea udhalilishaji huo.

NYOTA TISA HATARINI KUKOSA FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA.

JUMLA ya wachezaji tisa wako hatarini kukosa mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutokana na kuwa na kadi za njano kuelekea katika mchezo wa mkondo wa pili wa michuano hiyo. Kwa upande wa mabingwa watetezi Bayern Munich, mshambuliaji wao Mario Mandzukic yuko hatarini kufungiwa kucheza fainali ya michuano hiyo wakati watakapojitupa uwanjani kesho kujaribu kubadilisha matokeo ya kufungwa bao 1-0 na Real Madrid katika mchezo wa kwanza. Madrid wenyewe wana wachezaji watatu ambao wanaweza kukosa fainali hiyo itakayofanyika jijini Lisbon kama wakipewa kadi za njano katika mchezo huo utakaofanyika Ujerumani ambao ni Sergio Ramos, Xabi Alonso na Asier Illarramendi. Chelsea itaikaribisa Atletico Madrid katika mchezo wa maruadiano huku nyota wake wawili wa Kibrazil David Luiz na Willian wote wakiwa katika hatari kama hiyo ya kufugiwa mechi moja kama wakipewa kadi za njano katika mchezo huo. Atletico kama ilivyo kwa mahasimu wao Madrid nao wana wachezaji watatu waliokuwepo katika hatari hiyo ambao ni mabeki Emiliano Insua na Juanfran pamoja na kiungo Koke huku nahodha wao Gabi akiukosa mchezo wa marudiano kutokana na kuwa na kadi mbili za njano tayari.

MOURINHO ALIPAKI MABASI MAWILI - RODGERS.

MENEJA wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers amemtuhumu meneja wa Chelsea Jose Mourinho kwa kupaki mabasi mawili na kuipa ushindi wa mabao 2-0 katika Uwanja wa Anfield. Katika mchezo huo mabao ya Chelsea yalifungwa na Demba Ba aliyetumia vyema makosa ya nahodha Steven Gerrard kipindi cha kwanza na lingine la Willian katika majeruhi. Rodgers amesema wapinzani wao walipaki mabasi mawili langoni mwao akimaanisha walikuwa wakizuia kipindi chote cha mchezo huo hivyo kuwapa wakati mgumu kupenya ngome yao ingawa walijitahidi kujaribu. Rodgers amesema walijitahidi kushinda mchezo huo lakini walishindwa kupenya ngome ya wapinzani wao ambayo ilikuwa ikilindwa vizuri. Pamoja na ushindi huyo Mourinho bado ameendelea kudai kuwa hawana nafasi ya kunyakuwa ubingwa wa Ligi Kuu na kudai kuwa mbio hizo wamewaachia Manchester City na Liverpool. Mourinho amesema kitu cha msingi alichokuwa akihitaji ni kupata alama tatu hizo muhimu ambazo zitawasaidia kujihakikishia nafasi tatu katika masimama wa ligi hivyo kufuzu moja kwa moja bila kucheza mechi za mtoano katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

KUMPA GIGGS KIBARUA CHA KUINOA UNITED NI SAWA NA KUCHEZA KAMARI - BERG.

BEKI wa zamani wa Manchester United, Henning Berg anaamini itakuwa ni sawa na kucheza kamari kumteua Ryan Giggs kama meneja wa kudumu wa klabu hiyo. Kufuatia kutimuliwa kwa David Moyes Jumanne iliyopita, Giggs mwenye umri wa miaka 40 amekuwa akishikilia kwa muda kibarua hicho mpaka mwishoni mwa msimu, wakati Louis van Gaal akiaminika kukubali kutua Old Trafford baada ya mkataba wake na timu ya taifa ya Uholanzi kumalizika kiangazi hiki baada ya Kombe la Dunia. Giggs katika mechi yake ya kwanza ameiongoza United kuichabanga Norwich kwa mabao 4-0 mwishoni mwa wiki iliyopita lakini Berg anaamini nguli huyo bado anahitaji kocha mzoefu ili aweze kumsaidia. Berg amesema anaamini Giggs anaweza kuwa meneja mzuri huko mbele lakini kwasasa hana uzoefu anahitaji mtu mwenye uzoefu aweze kumsaidia.

SUAREZ, HAZARD WAZIKWAA TUZO UINGEREZA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Liverpool, Luis Suarez ametunukiwa tuzo ya kuwa mchezaji bora wa mwaka nchini Uingereza katika sherehe zilizofanyika jijini London jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay, mwenye umri wa miaka 27 alisafiri kuelekea kwenye sherehe hizo baada ya Liverpool kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Chelsea mapema jana. Akihojiwa mara baada kukabidhiwa tuzo hiyo, Suarez amesema Ligi Kuu imejaa wachezaji wengi bora hivyo ni heshima kubwa kwake kwa wachezaji hao kukumbuka mchango wake ndani ya uwanja. Nyota wa Chelsea Eden Hazard yeye alichaguliwa kuwa mchezaji bora chipukizi wa mwaka katika tuzo hizo ambazo huandaliwa na Chama cha Wachezaji wa Kulipwa nchini Uingereza.

Saturday, April 26, 2014

ULIMWENGU WA SOKA WAOMBOLEZA KIFO CHA TITO VILANOVA.

ULIMWENGU wa soka mwishoni mwa wiki hii umeamka na majonzi makubwa kufuatia kifo cha meneja wa zamani wa Barcelona Tito Vilanova kilichotokea jana. Vilanova amekuwa akipambana na maradhi ya saratani lakini taarifa za kifo chake zimeonyesha kumshitua na ghafla kwa kila mtu wakiwemo nyota wengi wa Barcelona. Rais wa klabu hiyo Josep Maria Bartomeu katika salamu zake za rambirambi amemuelezea Vilanova kama mkufunzi ambaye ameondoka lakini hawezi kusahaulika kamwe kutokana na ushujaa wake. Salamu zingine za rambirambi zimeendelea kumiminika kutoka kwa wachezaji wa Barcelona akiwemo Andres Iniesta, Xavi, Lionel Messi, Cesc Fabregas na wengineo. Katika salamu wengi wao wameonyesha kukumbuka mengi aliyoyafanya kocha huyo toka akiwa mwalimu katika shule ya soka ya Barcelona iitwayo La Masia mpaka alipopanda na kuwa kocha mkuu. Vilanova amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 45, na kuacha watoto wawili na mke baada ya kushindwa mapambano na saratani ya koo aliyopata toka mwaka 2011.


MICHUANO YA KAGAME KUANDALIWA KWA KAGAME MWENYEWE, ETHIOPIA WAPEWA CHALENJI.

BARAZA la Michezo la Nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA limeiteua Rwanda kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Kagame itakayofanyika Agosti mwaka huu wakati Ethiopia wenyewe wameteuliwa kuandaa michuano ya Chalenji inayotarajiw akufanyika kati ya Novemba na Desemba. Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye amesema kuwa wameichagua Rwanda kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ili kuadhimisha pamoja nao miaka 20 ya mauaji ya kimbari. Katika michuano ya mwaka jana klabu ya Vital’O ya Burundi ndio walikuwa mabingwa wa michuano hiyo iliyofanyika huko Darfur, Sudan. Yanga waliokuwa mabingwa wa michuano hiyo mwaka 2012 walishindwa kutetea taji lao mwaka jana baada ya kuamua kujitoa sambamba na Simba kutokana na masuala ya kiusalama nchini Sudan.

Friday, April 25, 2014

NAJIVUNIA KUINOA UNITED - GIGGS.

KOCHA wa muda wa klabu ya Manchester United, Ryan Giggs amesema kuifundisha timu hiyo ni moja ya matukio ya kujivunia katika maisha yake. Giggs raia wa Wales mwenye umri wa miaka 40 anategemewa kuingoza klabu hiyo katika mechi nne zilizobakia baada ya David Moyes kutimuliwa. Giggs ambaye ametumia maisha yake yote ya kucheza soka na sasa kocha wa muda akiwa na timu hiyo, anataka kuihakikishia klabu hiyo nafasi ya kushiriki michuano ya Europa League msimu ujao ambayo kwasasa inashikilia nafasi ya saba katika msimamo wa ligi. Akihojiwa katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari akiwa kocha leo, Giggs amesema anajisikia fahari na furaha kuifundisha klabu hiyo aliyoitumikia toka akiwa kijana mdogo.

SCOLARI ADOKEZA KIKOSI CHAKE.

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luiz Felipe Scolari amemuongeza Thiago Silva, David Luiz na Fred katika orodha yake ndogo ya wachezaji atakaowajumuisha katika kikosi chake cha Kombe la Dunia. Brazil inatarajiwa kuanza kampeni zake za kutafuta taji lake la sita wakati michuano hiyo takaporejea nchini humo katika majira ya kiangazi mwaka huu. Scolari amesema Silva, Luiz na Fred wana uhakika wa kuwepo katika kikosi chake cha kitakachokuwa na wachezaji 23. Kocha huyo amesema hao ndio wachezaji wake viongozi na tayari ameshazungumza nao zaidi katika safari zao, hana shaka kuhusu orodha yake ya mwisho lakini atasubiri mpaka mwishoni mwa msimu ligi zitakapomalizika. Scolari anatarajia kuteua kikosi kamili kwa ajili ya michuano hiyo Mei 7 mwaka huu.

RWANDA KUANDAA KAGAME, CHALENJI WAPEWA ETHIOPIA.

BARAZA la Michezo la Nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA limeiteua Rwanda kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Kagame itakayofanyika Agosti mwaka huu wakati Ethiopia wenyewe wameteuliwa kuandaa michuano ya Chalenji inayotarajiw akufanyika kati ya Novemba na Desemba. Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye amesema kuwa wameichagua Rwanda kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ili kuadhimisha pamoja nao miaka 20 ya mauaji ya kimbari. Katika michuano ya mwaka jana klabu ya Vital’O ya Burundi ndio walikuwa mabingwa wa michuano hiyo iliyofanyika huko Darfur, Sudan. Yanga waliokuwa mabingwa wa michuano hiyo mwaka 2012 walishindwa kutetea taji lao mwaka jana baada ya kuamua kujitoa sambamba na Simba kutokana na masuala ya kiusalama nchini Sudan.

FA YATUMA MAOMBI YA WEMBLEY KUWA MWENYEJI WA EURO 2020.

CHAMA cha Soka nchini Uingereza-FA kimepeleka maombi ya Uwanja wa Wembley kuwa mwenyeji wa aidha nusu fainali na fainali ya michuano ya Euro 2020 au baadhi ya mechi za makundi. Maombi hayo yametumwa katika dakika za mwisho kabla ya muda wa mwisho kufanya hivyo wakati Wales na Scotland pia zimeomba uenyeji wa mechi za makundi. Ilitangazwa Desemba mwaka jana kuwa michuano hiyo ya Ulaya inatarajiwa kuandaliwa na miji mbalimbali kuzunguka bara hilo. Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA linatarajia kutangaza miji 13 itakayokuwa mwenyeji wa michuano hiyo katika sherehe zitakazofanyika Septemba 19 mwaka huu.

Thursday, April 24, 2014

BELUSCONI AGOMA KUUZA AC MILAN.

MAOFISA wa AC Milan wamebainisha kuwa hakuna mpango wa kuuza klabu hiyo, pamoja na tetesi ya kutaka kununuliwa na mfanyabiashara wa Singapore Peter Lim. Vyombo vya habari nchini Italia vimedai kuwa bilionea huyo mwekezaji ametoa ofa ya euro milioni 500 kwa ajili ya kununua hisa nyingi za klabu hiyo. Mbali na Lim, kuna taarifa zingine zinazodai kuwa mfanyabiashara mwingine kutoka China Zong Qinghou pia anaangalia uwezekano wa kuinunua timu hiyo. Hata hivyo, mwenyekiti wa klabu hiyo Silvio Belusconi alikanusha tetesi hizo na kudai kuwa hana mpango kuachia umiliki kwenda kwa yoyote. Belusconi ndio anaemiliki hisa nyingi katika klabu hiyo.

STURRIDGE FITI KUIVAA CHELSEA.

MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Daniel Sturridge anategemewa kurejea kutoka katika majeruhi katika mchezo wa Jumapili ambao watakwaana na Chelsea. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye miaka 24 alikuwa akilalamika maumivu ya msuli katika ushindi wa mabao 3-2 waliopata dhidi ya Manchester City Aprili 13 hivyo kupelekea kutolewa nje. Toka apate majeruhi hayo alikosa mechi moja lakini sasa anategemewa kurejea tena uwanjani kuisaidia Liverpool katika mchezo huo muhimu ambao kama wakishinda utawafanya kuendelea kujikita kileleni hivyo kuweka hai matumaini yao ya ubingwa wa Ligi Kuu. Sturridge amesema kwasasa anajisikia vyema na ni mategemeo yake atakuwepo katika mchezo huo wa Jumapili lakini itategemea kama kocha Brendan Rodgers atamchagua.

PLATINI AZIKINGIA KIFUA PSG NA MAN CITY.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya, Michel Platini amesisitiza kuwa Paris Saint-Germain-PSG na Manchester City hazitafungiwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kama wakikutwa na hati ya kukiuka sheria ya matumizi ya fedha. Bodi ya UEFA inayosimamia sheria hiyo imekutana mapema mwezi huu kufanya uchunguzi wa timu zilizokiuka sheria hiyo ambapo mbali na PSG na City vipo pia vilabu vingine 76. Bodi hiyo inatarajiwa kutangaza matokeo ya uchunguzi wake mapema mwezi ujao lakini Platini tayari ameweka wazi kuwa PSG na City hazitaondolewa katka michuano hiyo. Platini amesema kutakuwa na adhabu kali kwa timu zilizokiuka sheria hiyo lakini hakuna yoyote itakayoondolewa katika michuano ya Ulaya.

HATIMAYE JANUZAJ ACHAGUA KUITUMIKIA UBELGIJI.

WINGA wa klabu ya Manchester United, Adnan Januzaj ameamua kuiwakilisha Ubelgiji katika michuano ya soka ya kimataifa. Kocha wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Marc Wilmots ametangaza katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter amefurahishwa na uamuzi uliochukuliwa na mchezaji huyo. Januzaj amezaliwa jijini Brussels akiwa na wazazi wenye asili ya Kosovo na Albania na kujiunga na United mwaka 2011. Kinga huyo mwenye umri wa miaka 19 alikuwa na nafasi ya kuzichezea nchi za Kosovo, Albania, Turkey, Serbia na hata Uingereza lakini sasa anaweza kuwemo katika kikosi cha Ubelgiji kitakachoshiriki Kombe la Dunia. Kikosi kamili cha wachezaji 30 wa Ubelgiji kinatarajiwa kutajwa Mei 13 mwaka huu.

ARSENAL NAO WAMUWINDA LOUIS VAN GAAL.

KLABU ya Arsenal imefanya mawasiliano na Louis van Gaal kutokana na kutokuwa na uhakika na mstakabaliwa kocha Arsene Wenger. Arsenal bado wana matumaini kuwa Wenger atasaini mkataba mpya wa miaka miwili waliokubaliana Octoba mwaka jana lakini inajulikana anaweza kujiuzulu kama akishindwa kufikia malengo aliyojiwekea baada ya kumalizika kwa msimu. Imebainika kuwa Mfaransa huyo aliwaambia marafiki zake kuwa anafikiria kuacha kuinoa Arsenal kama awatashinda Kombe la FA na kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu. Kutokana na hali hiyo kumekuwa na mipango ya muda mfupi inayofanywa na Arsenal, mojawapo ni kujaribu kufanya mazungumzo na Van Gaal ambaye mkataba wake na timu ya taifa ya Uholanzi unamalizika baada ya Kombe la Dunia. Mbali na kuwindwa na Arsenal, Van Gaal pia anawindwa na Manchester United na Tottenham Hotspurs ambao nao wanataka achukue nafasi ya Tim Sherwood mwishoni mwa msimu huu.

ROBBEN AISHANGAA BAYERN.

WINGA mahiri wa klabu ya Bayern Munich, Arjen Robben ameshangawa na mchezo wa tahadhari waliokuwa wakicheza Real Madrid katika mchezo wao wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Pamoja na Madrid kushinda bao 1-0 katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, Bayern ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo walimiliki sehemu kubwa ya mchezo huo kwa asilimia 72. Akihojiwa Robben amesema alitegemea mengi zaidi kutoka kwa Madrid lakini badala yake walikuwa wakiwasubiri na kuwaacha watawale mchezo. Katika mchezo huo Karim Benzema ndiye aliyefunga bao pekee lakini ilibakia kidogo Mario Gotze na Thomas watasawazishe baada ya kukosa kufunga katika nafasi za wazi walizopata. Timu hizo zinatarajiwa kurudiana tena Jumanne ili kutafuta mshindi atakayekwenda kwenye fainali itakayofanyika jijini Lisbon, Ureno.

JUVENTUS, BENFICA HAPATOSHI EUROPA LEAGUE.

BAADA ya kumalizika kwa mechi za mkondo wa kwanza za nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa jana, leo kuna uhondo mwingine wa michuano ya Europa League ambapo viwanja viwili vitawaka moto. Katika mechi za leo Juventus maarufu kama vibibi watakua ugenini kupepetana na Benfica ya Ureno katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali. Nusu fainali nyingine ya michuano hiyo inatarajiwa kuzikutanisha timu za Hispania ambapo Sevilla watakuwa nyumbani kuwakaribisha Valencia. Fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kupigwa huko jijini Turin katika Uwanja wa Juventus Mei 14 mwaka huu.

Wednesday, April 23, 2014

BAADA YA KUKAA NJE KWA MIEZI 13 HATIMAYE DIABY AREJEA TENA UWANJANI.

KIUNGO Abou Diaby amerejea uwanjani kwa mara ya kwanza baada ya kukaa nje kwa zaidi ya mwaka wakati alipocheza kwa dakika 45 katika kikosi cha Arsenal cha vijana chini ya mri wa miaka 21 waliocheza na Chelsea. Mara ya mwisho kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 kuonekana uwanjani ilikuwa ni Machi 27 mwaka jana katika mchezo dhidi ya Swansea City ambapo aliumia msuli wa ndani ya goti. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amedokeza kuwa kurejea uwanjani kwa nyota huyo kunaweza kuwa dalili njema za kurejea katika kikosi cha kwanza. Wenger amesema Diaby hajacheza soka kwa kipindi cha mwaka mzima lakini kimwili yuko tayari kucheza, kwasasa ni suala la maamuzi na anahitaji mechi nyingi zaidi ili aweze kuzoea changamoto kwa tena.

MOURINHO KUWAPUMZISHA NYOTA WAKE KATIKA MCHEZO DHIDI YA LIVERPOOL.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amesema anataka kuwapumzisha nyota wake kwa ajili ya safari kwenda Anfield kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Liverpool Jumapili ijayo. Chelsea bado bado wako katika kinyang’anyiro cha taji la ligi wakiwa wamebakiwa na michezo mitatu lakini Mourinho anataka kuhamishia nguvu zake katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid. Hata hivyo, kocha huyo amesema uamuzi huyo wa kuwapumzisha baadhi ya nyota wake unaweza usiwe wa kwake kuufanya kwasababu anataka kusikiliza na mawazo ya wengine. Kipigo cha mabao 2-1 walichopata Chelsea kutoka kwa Sunderland mwishoni mwa wiki iliyopita kinamaanisha hata kama wakishinda mchezo wa Anfield inaweza isitoshe kuizuia Liverpool kushinda taji la ligi baada ya kupita miaka 24.

FIFA YIRUHUSU BARCELONA KUSAJILI MPAKA RUFANI YAO ITAKAPOSIKILIZWA.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetangaza kuwa Barcelona itaruhusiwa kusajili wachezaji katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi baada ya kuamua kuisimamisha adhabu waliyopata kufuatia rufani waliyokata. Barcelona walikuwa wamefungiwa kufanya usajili kwa simu mmoja kutokana na kukiuka sheria za usjaili wa kimataifa kwa wachezaji walio na umri chini ya miaka 18 lakini adhabu hiyo imetenguliwa ikisubiri uamuzi wa mwisho katika rufani yao utakapotolewa. FIFA imefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa kamati yake ya rufani haiwezi kukutana katika kipindi hiki cha karibuni kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa Julai mosi mwaka huu. Uamuzi huo unamaanisha klabu hiyo inaweza kuendelea na taratibu zake za usajili majira ya kiangazi ikiwa tayari imeshamsajili kinga Alen Halilovic kutoka Dinamo Zagreb huku wakiwa mbioni kukamilisha usajili wa golikipa wa Borussia Monchengladbach Marc-Andre ter Stegen.

KUFUZU LIGI YA MABINGWA ULAYA ITATUSAIDIA KATIKA USAJILI - AYRE.

MKURUGENZI mtendaji wa Liverpool, Ian Ayre amesema kufuzu kwa klabu hiyo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutawasaidia sana katika usajili majira ya kiangazi. Ushindi wa mabao 3-2 waliopata Liverpool dhidi ya Norwich City Jumapili iliyopita, umeithibitishia timu hiyo kumaliza katika nafasi tatu za juu na kuwafanya kurejea katika michuano hiyo toka mwaka 2009. Ayre amekiri timu kushindwa kufuzu michuano hiyo kipindi cha nyuma ilikuwa inawapa wakati mgumu kuzungumza na wachezaji. Bosi huyo amesema kipindi cha usajili hali ilikuwa ngumu akitolea mfano wlaipopata tabu kumshawishi Luis Suarez kubaki Liverpool kwasababu alikuwa akitaka kucheza katika michuano hiyo dhidi ya wachezaji bora. Lakini kwa mafanikio waliyopata safari hii ya kufuzu michuano hiyo huku wakiwa katika nafasi nzuri ya kunyakuwa taji la ligi kwa mara ya kwanza toka mwaka 1990, Ayre anaamini mazungumzo katika kipindi cha usajili yatakuwa rahisi kutokana na nafasi waliyonayo.

MBINU CHAFU ZA MOURINHO ZAMKERA SUAREZ.

KIUNGO wa klabu ya Atletico Madrid, Mario Suarez ameeleza kuchukukizwa kwake na mbinu zisizo sahihi zilizokuwa zikitumiwa na Chelsea katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya timu hizo. Suarez amesema anadhani wakongwe hao wa Ligi Kuu nchini Uingereza walikwenda katika Uwanja wa Vicente Calderon kwa dhumuni moja la kutafuta sare. Atletico wanaonolewa na Diego Simeone walimiliki mpira sehemu kubwa ya mchezo huo uliochezwa jana usiku lakini walishindwa kuipenya safu ya ulinzi ya Chelsea hivyo kusababisha timu hizo kutoka sare ya bila kufungana. Kiungo huyo amesema Chelsea wamepata walichokuwa wakikitaka yaani sare lakini bado wana mchezo wa marudiano hivyo anadhani bado wana nafasi.

FERGUSON ALIKUWEMO KATIKA KIKAO CHA KUMTIMUA MOYES.

MENEJA wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson anatarajiwa kuwa sehemu muhimu katika kutafuta mbadala wa David Moyes katika timu hiyo. Safari hii Ferguson aakuwa sambamba na wajumbe wote wa bodi ya klabu hiyo katika uchaguzi wa kocha mpya. Bodi hiyo ilikutana baada ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka Everton Jumapili iliyopita kuzungumzia hatua ya kumfukuza Moyes na Ferguson pamoja na nguli wa zamani wa klabu hiyo Sir Bobby Charlton inaaminika walikuwemo katika kikao hicho. Ryan Giggs ndio aliyepewa mikoba ya kuinoa United kwa muda mpaka atakapopatikana kocha mpya lakini inaaminika kuwa mkongwe huyo hayupo katika orodha ya makocha watakaofanyiwa usaili.

TERRY, CECH WASHINDWA KUMALIZIA MSIMU.

NAHODHA wa Chelsea John Terry na golikipa Petr Cech wanatarajiwa kukosa mechi za Ligi Kuu zilizosalia baada ya kupata majeruhi katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid jana. Terry alitolewa nje kwa matatizo ya mguu wakati Cech yeye alijumiza bega lake katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana. Meneja wa Chelsea, Jose Mourinho amesema Terry anaweza kucheza tena kama timu hiyo itafanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo itakayofanyika Mei 24 mwaka huu. Ligi Kuu nchini Uingereza inatarajiwa kufunga pazia lake Mei 11 mwaka huu.

Tuesday, April 22, 2014

VAN GAALA APEWA NAFASI YA KUCHUKUA MIKOBA YA MOYES BAADA YA KLOPP KUCHOMOA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal ameonyesha nia ya kutaka kuchukua mikoba ya David Moyes kama meneja mpya wa Manchester United. Mholanzi huyo aliwatonya marafiki zake kuwa anatamani kutua Old Trafford wakati mkataba wake wa kuinoa nchi hiyo utakapomalizika baada ya michuano ya Kombe la Dunia. Kumekuwa na ripoti zilizodai kuwa Van Gaal alikutana na ujumbe wa United wiki iliyopita na mazungumzo zaidi yanatarajiwa kuendelea wakati United itakapoanza hatua ya kutafuta mbadala wa Moyes. Jurgen Klopp pia aifuatwa na United lakini meneja huyo wa Borussia Dortmund alitangaza kutokuwa na mpango wa kuinoa United mapema leo. Klopp alikaririwa akidai kuwa United ni klabu kubwa na anajiona kuwa karibu na mashabiki wake lakini hawezi kuondoka Dortmund kwasasa.

DORTMUND HAITAYUMBA KWA KUONDOKA KWA LEWANDOWSKI - WATZKE.

OFISA mkuu wa klabu ya Borussia Dortmund, Hans-Joachim Watzke amedai kuwa meneja Jurgen Klopp atahakikisha timu hiyo haitetereki kutokana na pengo la kuondoka kwa Robert Lewandowski. Nyota huyo wa kimataifa wa Poland ambaye alifikisha mabao 100 katika klabu hiyo kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Ujerumani dhidi ya Wolfsburg, atajiunga na Bayern Munich kwa uhamisho huru mwishoni mwa msimu huu. Hata hivyo, pamoja na kuondoka kwa mshambuliaji huyo, Watzke anaamini kuwa timu hiyo haitayumba kwani Klopp mara zote amekuwa akitafuta njia mbadala pindi anapoondokewa na nyota wake kama ilivyokuwa kwa Nuri Sahin aliyekwenda Real Madrid na Shinji Kagawa aliyekwenda Manchester United. Bosi huyo amesema anajua hawawezi kuziba la Lewandowski kama yeye lakini anajua pia hawawezi kuyumba kwasababu ya kuondoka kwake.

KIINGILIO CHA CHINI TAIFA STARS NA BURUNDI 5,000.

SHIRIKISHO la Soka nchini-TFF limetaja viingilio vya mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Taifa Stars na timu ya taifa ya Burundi unaotarajiwa kuchezwa Aprili 26 mwaka katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katika taarifa iliyotumwa katika vyombo vya habari na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, imedai kuwa mchezo utakuwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa kiingilio cha chini katika mchezo huo kitakuwa shilingi 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP A kiingilio kitakuwa 20,000 huku VIP B na C kiingilio kitakuwa 10,000. Taifa Stars kwasasa wako kambini katika hoteli ya Kunduchi Beach tayari kujiandaa na mchezo huo huku wapinzani wao Brundi wakiwa wametua nchini leo kwa ajili ya mechi hiyo ya kusisimua.

MCHEZAJI AFARIKI KWA KUKANYAGWA HUKO GABON.

GOLIKIPA wa timu ya AC Bongoville, Sylvain Azougoui amefariki dunia baada ya kukanyagwa kichwani wakati wa mchezo wa ligi huko nchini Gabon. Golikipa huyo alifariki wakati akikimbizwa hospitali baada ya tukio hilo wakati wa mechi dhidi ya timu ya Centre Mberi Sportif. Azougoui mwenye umri wa miaka 30 raia wa Togo, alikuwa amezuia shuti lililokwenda langoni mwake lakini mshambuliaji aliyepiga shuti hilo alipoteza mwelekeo katika nyasi zilizokuwa zimelowa na kumkanyaga golikipa huyo kichwani. Klabu hiyo ilithibitisha habari za kifo cha golikipa huyo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook na kueleza masikitiko yake kwa pengo aliloacha klabuni na kwa familia yake.

SIKUPENDA KUPANGWA NA REAAL MADRID - MARTINEZ.

KIUNGO wa klabu ya Bayern Munich, Javi Martinez amekiri hakutaka timu yake ipangwe kuchuana na Real Madrid katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mabingwa hao watetezi wa michuano hiyo wanatarajiwa kupepetana na Madrid katika mchezo wa mkondo wa kwanza utakaochezwa kesho ambao utakuwa ni kama marudiano ya nusu fainali ya mwaka 2012 ambayo Bayern walivuka kwa changamoto ya mikwaju ya penati. Martinez anaamini kuwa Madrid ni timu ngumu pekee iliyobakia katika michuano hiyo ambayo itabidi wapambane nayo na kuwaonya wachezaji wenzake kuwa makini kama wanataka kutetea taji lao. KIungo aliendelea kudai kuwa Madrid ni timu ambayo inakuwa siku hadi siku huku wakiwa na wachezaji nyota kama Angel Di Maria, Gareth Bale na Cristiano Ronaldo ambao wanaweza kuleta madhara wakati wowote unapocheza nao.

ETO'O KUIKOSA ATLETICO MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Chelsea Samuel Eto’o anatarajiwa kuukosa mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhhidi ya Atletico Madrid kutokana na majeruhi ya goti. Nyota huyo ameshindwa kusafiri na kikosi cha timu hiyo kilichoelekea nchini Hispania kwa ajili ya mchezo na vinara hao wa La Liga utakaochezwa baadae leo. Eto’o aliifungia bao Chelsea wakati ilipokubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Sunderland Jumamosi iliyopita lakini alitolewa baada ya dakika 74 za mchezo. Hata hivyo, Eden Hazard ameanza mazoezi kufuatia majeruhi yaliyokuwa yakimsumbua na kumfanya kukaa nje kwa wiki mbili. Kukosekana kwa Eto’o, Mourinho anaweza kumchagua Fernando Torres ambaye aliondoka Atletico mwaka 2007 kujiunga na Liverpool kuziba nafasi hiyo.

NEYMAR ANAIWAZA ZAIDI BARCELONA KULIKO KOMBE LA DUNIA - BABA.

BABA wa mshambuliaji nyota wa Barcelona, Neymar amedai kuwa mwanae anafanya jitihada za kurejea uwanjani kuitumikia klabu yake na sio michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika katika majira ya kiangazi. Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil kwasasa yuko nje ya uwanjani akijiuguza majeruhi ya mguu wake wa kushoto aliyopata katika fainali ya Kombe la Mfalme, ambapo atakuwa nje kwa kipindi cha wiki nne. Neymara alikaririwa wiki iliyopita akidai kuwa ana malengo ya kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa Barcelona dhidi ya Atletico Madrid, baada ya kukiri kuwa anahofu juu ya matumaini yake ya kucheza Kombe la Dunia. Hata hivyo, baba yake amesema mwanae huyo kwasasa anafikiria kurejea katika kikosi cha kwanza cha Barcelona halafu baada ya hapo ndio atafikiria michuano hiyo itakayofanyika katika ardhi ya nyumbani kwao Brazil. Neymar amefunga mabao 15 katika mechi 40 alizoichezea Barcelona katika mashindano yote msimu huu.

CITY BADO HAWAJAKATA TAMAA NA UBINGWA - KOMPANY.

BEKI wa klabu ya Manchester City, Vincent Kompany amesema ushindi wa dakika za mwisho waliopata na kunyakuwa taji la Ligi Kuu 2012 ndio unaowapa matumaini kuelekea katika michezo yao minne iliyobakia. Ushindi wa mabao 3-1 iliyopata City dhidi ya West Bromwich Albion jana usiku umeifanya timu hiyo kupunguza pengo la alama na vinara Liverpool kufikia sita huku wakiwa wamebakiwa na mechi moja mkononi. City walinyakuwa taji lao la kwanza la ligi baada ya miaka 44 mwaka 2012, kwa mabao mwili yaliyofungwa katika dakika za majeruhi katika mechi ya mwisho wa msimu na Kompany ambaye pia ni nahodha wa timu hiyo anaamini chochote kinaweza kutokea katika mechi zilizobakia. Kompany amesema hataki kukata tamaa kwasababu mwaka 2012 walitawadhwa mabingwa katika mchezo wa mwisho tena dakika za lala salama hivyo haoni kwanini hilo lishindikane safari kwasababu bado mechi nne kabla msimu haijamalizika.

HATIMAYE UNITED WAMTIMUA MOYES RASMI.

HATIMAYE klabu ya Manchester United imemtupia virago meneja wake David Moyes baada ya wamiliki wake familia ya Glazer kumchoka kocha huyo raia wa Scotland. Moyes mwenye umri wa miaka 50, ambaye amejitengenezea rekodi zisizihitajika Old Trafford anakuwa meneja wa kwanza wa United kutimuliwa toka Ron Atkinson mwaka 1986. Klabu hiyo ilitangaza kumtimua Moyes katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter ambapo pia walimshukuru kwa juhudi zake katika kipindi chote cha miezi 10 alichoinoa timu hiyo. Moyes alichaguliwa na Sir Alex Ferguson kuchukua nafasi yake wakati kocha huyo alipostaafu msimu uliopita baada ya kuinoa timu hiyo kwa misimu 26. Mkongwe Ryan Giggs atachukua mikoba kama kocha wa muda wakati klabu ikitafuta mbadala wa Moyes, ambapo majina kama Jurgen Klopp, Louis van Gaal na Carlo Ancelotti yanapewa nafasi ya kuziba pengo hilo.

Sunday, April 20, 2014

HAPPY EASTER WASOMAJI WOTE WA BEKI3.BLOGSPOT.COM.

BEKI3 inawatakia wasomaji wake wapendwa wa heri ya sikukuu ya Pasaka.

WENGER AMTOA HOFU HODGSON KUHUSU HALI YA WILSHERE.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amempa taarifa njema kocha wa timu ya taifa ya Uingereza Roy Hodgson kuwa Jack Wilshere atakuwa fiti kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 12 mwaka huu. Wilshere mwenye umri wa miaka 22 alikuwa amekaa nje ya uwanja toka alipoumia mguu akiitumikia timu ya taifa Machi 5 mwaka huu. Hodgson anatarajia kutaja kikosi cha wachezaji 30 kwa ajili ya michuano hiyo Mei 13 na Wenger amesema amemuhakikishia kuwa Wilshere atakuwa fiti ikifika wakati huo. Wenger amesema nyota huyo ameanza mazoezi kukimbia wiki hii hivyo anadhani baada ya wiki mbioi au tatu atakuwa ameshakuwa fiti tayari kwa kurejea uwanjani. Kupona kwake pia kutamfanya ajumuishwe katika kikosi cha Arsenal kitakachoivaa Hull City katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA Mei 17 katika Uwanja wa Wembley.