Friday, October 24, 2014

VILABU ULAYA VYAITAKA FIFA KUKUBALI KOMBE LA DUNIA 2022 KUCHEZWA MEI.

VILABU vikubwa barani Ulaya vinatarajia kulitaka Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kucheza michuano ya Kombe la Duniani mwaka 2022 nchini Qatar katika kipindi cha mwezi Mei. Qatar ilishinda haki za kuandaa michuano hiyo mwaka 2010 lakini mjadala wa kuhamisha michuano hiyo kutoka katika majira ya kiangazi kama ilivyozoeleka umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya mwaka. Chama cha Vilabu Ulaya-ECA ambacho kinajumuisha klabu za Manchester United, Liverpool, Barcelona na Bayern Munich vimejadili kuwa kipindi cha mwezi Mei mwaka 2022 kitakuwa muafaka kwa michuano hiyo. ECA wanaamini michuano hiyo kuchezwa katika kipindi cha majira ya machipuko kitasaidia kupunguza hatari iliyopo ya kucheza katika joto kali. Maswali yaliibuka haraka baada ya Qatar kupata haki ya kuandaa michuano hiyo kuhusu uwezekano wake kutokana na joto kali lililopo katika nchi hiyo ya jangwa katika kipindi June na Julai ambacho ndio Kombe la Dunia huchezwa. Ila mara zote Qatar wenyewe wamekuwa wakisisitiza wanaweza kuandaa michuano hiyo kiangazi kwa kutumia mpango wao wa vipoza hewa ili kupunguza joto nmdani ya viwanja na sehemu ambazo zitakuwa zimetengwa kwa ajili ya mashabiki.

No comments:

Post a Comment