Wednesday, September 17, 2014

MAN UNITED HAWANA UWEZO WA KUNUNUA NYOTA WA BAYERN - GUARDIOLA.

MENEJA wa klabu ya Bayern Munich, Pep Guardiola ametamba kuwa Manchester United hawana uwezo wa kuwanasa wachezaji wake. United imetumia zaidi ya paundi milioni 150 katika usajili wa kiangazi baada ya kushindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ukiwemo usajili uliovunja rekodi nchini Uingereza kwa kitita cha paundi milioni 59.7 kwa ajili ya Angel Di Maria kutoka Real Madrid. Lakini Guardiola ametamba kuwa hakuna nyota wake anayeweza kwenda Old Trafford kwani klabu hiyo haina fedha za kutosha. Akihojiwa kabla ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City baadae leo, Guardiola amesema ameona United wametumia fedha nyingi katika usajili hiyo ni sehemu ya mchezo lakini hadhani kama wataweza kuwashawishi wachezaji wake kwenda huko. Guardiola ambaye alikuwa katika kikosi cha Barcelona wakati ikinolewa na Louis van Gaal kabla ya yeye mwenyewe hajawa kocha, aliongeza kuwa kushindwa kwa United kufuzu michuano ya Ulaya kunaonyesha jinsi gani mchezo wa soka ulivyo wa kipekee.

No comments:

Post a Comment