Friday, July 31, 2015

CHELSEA VS ARSENAL NGAO YA JAMII JUMAPILI.

PAZIA la Ligi Kuu nchini Uingereza, linatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa wiki kwa mchezo wa Ngao ya Jamii utakaozikutanisha timu za Chelsea na Arsenal zote kutoka jijini London. Mchezo huo ambao utachezwa Jumapili hii katika Uwanja wa Wembley huzikutanisha timu ambazo ni mabingwa katika Ligi Kuu pamoja na Kombe la FA. Chelsea wao ndio waliibuka mabingwa wa ligi msimu uliopita huku Arsenal wao wakifanikiwa kutetea taji lao la FA kwa mara ya pili na kuweka historia kuwa timu ya kwanza kunyakuwa taji hilo mara nyingi zaidi. Ligi rasmi inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 8 mwaka huu kwa michezo nane ambapo Manchester United watakuwa wenyeji wa Tottenham Hotspurs katika Uwanja wa Old Trafford huku Bournemouth ambao wamepanda daraja msimu huu wao wakiikaribisha Ason Villa. Nyingine ni Norwich City watakaokuwa wenyeji wa Crystal Palace, Leicester City dhidi ya Sunderland, Everton dhidi ya Watford na mabingwa Chelsea dhidi ya Swansea City.

FENERBAHCE YAIKATIA RUFANI SHAKHTAR KWA KUMCHEZESHA FRED.

KLABU ya Fenerbahce imetuma malalamiko yake Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA baada ya Shakhtar Donetsk kumchezesha kiungo wa kimataifa wa Brazil Fred dhidi yao, pamoja na kukabiliwa na tuhuma za kutumia dawa za kusisimua misuli. UEFA imethibitisha kuwa inafanyia uchunguzi mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya tatu ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa Jumanne iliyopita na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2. Taarifa kutoka nchini Brazil zinadai kuwa Fred mwenye umri wa miaka 22, alikutwa na chembechembe za dawa hizo zilizopigwa marufuku wakati alipofanyiwa vipimo katika michuano ya Copa America iliyomalizika hivi karibuni huko Chile. Kocha wa Shakhtar Mircea Lucescu amekiri UEFA walimshauri kutomchezesha Fred katika mchezo huo. Mchezaji huyo atakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kama vipimo vya pili vitathibitisha kuwa alitumia dawa hizo.

CBF KUMUUNGA MKONO ZICO URAIS FIFA.

SHIRIKISHO la Soka la Brazil-CBF limetangza kumuunga mkono nguli wa soka wa nchi hiyo Zico (PICHANI) katika kinyang’anyiro cha urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA utakaofanyika Februari 26 mwakani. Rais wa CBF Marco Polo Del Nero amesema katika taarifa yake kuwa wanamuunga mkono Zico mwenye umri wa miaka 62 na kama atapata saini nne zinazohitajika hakuna shaka CBF watazipitisha. Ili Zico aweze kuwa mgombea rasmi wa kiti hicho anatakiwa aungwe mkono na mashirikisho ya soka kutoka nchi nne tofauti. Rais wa sasa Sepp Blatter alitangaza kuachia ngazi wadhifa wake huo Juni 2 mwaka huu ikiwa zimepita siku nne toka achaguliwe kuongoza kwa muhula wa tano kufuatia tuhuma za ufisadi zilizolikumba shirikisho hilo. Mbali na Zico wengine waliotangaza nia ya kuchukua nafasi hiyo ya Blatter, ni pamoja na rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Michel Platini.

VAN DER VAART AITUHUMU MADRID KWA KUKOSA UVUMILIVU.

KIUNGO wa zamani wa Real Madrid, Rafael van der Vaart ameituhumu klabu yake hiyo ya zamani wa kukosa uvumilivu. Kiungo huyo wa kimataifa wa Uholanzi alivaa jezi ya Madrid kuanzia mwaka 2008 mpaka 2010 kabla ya kuondoka na kuhamia Tottenham Hotspurs na anadhani mategemeo makubwa waliyonayo hayaisaidii timu hiyo. Akihojiwa Van der Vaart amesema ukiwa Madrid kama hutashinda chochote lazima utaingia katika matatizo makubwa. Mkongwe huyo aliendelea kudai kuwa kwa maono yake anadhani Madrid hawana uvumilivu kwani ukipoteza mechi moja kwao ni kama duniani inakuwa imeishia hapo.

JIJI LA BEIJING LAPEWA SHAVU LA WINTER OLIMPIKI.

JIJI la Beijing limechaguliwa kuwa mwenyeji wa michuano ya Olimpiki na Paralimpiki ya majira ya baridi wakiushinda mji wa Almaty ulioko Kazakhstan. Wakiwa wenyeji wa michuano ya olimpiki mwaka 2008, Beijing ambao ndio mji kuu wa China sasa unakuwa mji wa kwanza kuandaa michuano yote miwili ya majira ya kiangazi na baridi. Miji ya Beijing na Almaty haikuwa ikipewa nafasi wakati kinyang’anyiro cha kugombea nafasi hiyo kilipoanza miaka miwili iliyopita. Lakini baada ya miji kadhaa ya Ulaya kujitoa kutokana na sababu za kisiasa au kiuchumi, Beijing ilifanikiwa kuibuka kidedea kwa kuzoa kura 44 dhidi ya kura 40 za Almaty.

GUARDIOLA MGUU NDANI MGUU NJE BAYERN.

MENEJA wa Bayern Munich, Pep Guardiola amesema hatasaini mkataba mpya na klabu hiyo mpaka atakapojiridhisha kuwa ni jambo la busara kwa pande zote mbili. Kumekuwa na tetesi zilizoibuka juu ya mustakabali wa kocha huyo ambaye mkataba wake unamalizika mwakani huku taarifa zingine zikidai tayari ameshakubali kuhamia Manchester City. Guardiola mwenye umri wa miaka 44, hajathibitisha mipango yake lakini amekiri kuwa hana uhakika kama ataendelea kuwepo Allianz Arena. Akizungumza na wanahabari, Guardiola amesema kwasasa yeye ni kocha wa Bayern na anafurahia hilo lakini bado hajaamua kuhusu mustakabali wake na pindi atakapopata uamuzi atawaarifu Kalle Rummenigge ambaye ni rais, Mathias Sammer mkurugenzi wa michezo na Uli Hoeness ambaye ni rais wa zamani wa klabu hiyo.